ICC inachunguza mauaji ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria
Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu yenye makao yake London nchini Uingereza imesema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inaendelea kuchunguza mauaji ya halaiki ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria.
Katika taarifa, Islamic Human Rights Commission (IHRC) imesema Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC angali anaendelea kukusanya ushahidi ili kukamilisha mchakato wa kuwasilisha mbele ya majaji wa mahaka hiyo ya kimataifa faili la mauaji hayo ya kutisha dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria ya mwishoni mwa mwaka 2015.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague nchini Uholanzi ingali inasubiri taarifa muhimu kutoka serikali ya Abuja; huku Fatou Bensouda, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC akieleza wasiwasi wake kuwa kuna njama zinapikwa za kujaribu kupoteza au kupotosha ushahidi wa mauaji hayo.
Kwa mujibu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu, Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo la tarehe 13 Disemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussaynia ya Baqiyatullah na nyumba ya Sheikh Zakzaky.
Taasisi hiyo ya kutetea haki za binadamu ya mjini London kadhalika imeonya kuwa, hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa Kiislamu anayeshikiliwa gerezani imezidi kuwa mbaya, huku ikitoa mwito wa kuachiwa huru mwanazuoni huyo pamoja na mkewe Malama Zeenat kwa ajili ya kupewa matibabu ya dharura.
Oktoba mwaka jana, Islamic Human Rights Commission ilisema vyombo vya usalama vya Nigeria vinapanga njama za kuvuruga ushahidi sambamba na kuwaua mashahidi wa jinai hiyo ya kutisha ya Zaria ya Disemba 2015.