Ripoti: Waislamu, wahanga wakuu wa mashambulio ya al-Shabaab
Uchunguzi uliofanywa na shirika moja lisilo la kiserikali umefichua kuwa, Waislamu ndio wahanga wakuu wa mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab la Somalia, licha ya genge hilo kudai kuwa haliwalengi Waislamu na Wasomali katika hujuma zao.
Ripoti ya uchunguzi huo uliofanywa na taasisi ya Armed Conflict, Location and Event Data Project (ACLED) imebainisha kuwa, tangu kundi hilo lianzishe harakati zake nchini Somalia mwaka 2006, Waislamu hususan wenye asili ya Kisomali ndio walengwa wakuu wa mashambulio ya kila uchao ya kundi hilo ambalo lilijitangaza kuwa ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Kwa mujibu wa takwimu za ACLED, zaidi ya raia elfu nne wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi ya al-Shabaab tokeo mwaka 2010, aghalabu ya hujuma hizo zikishuhudiwa nchini Somalia.
Kundi hilo limekuwa likitekeleza pia mashambulizi ya hapa na pale katika nchi nyingine za Afrika Mashariki hususan nchini Kenya.
Mwezi uliopita, genge hilo la ukufurishaji kwa kutumia uzandiki na hadaa zake za kila uchao, liliwaomba radhi wananchi wa Somalia, eti kwa kuwaua 'kimakosa' makumi ya watu katika shambulizi la bomu mjini Mogadishu.
Kupitia msemaji wake Ali Dhere, genge hilo liliandika taarifa inayosema: "Tumefanya shambulio ambalo limesababisha kupotea kwa roho na mali za Waislamu. Tunaomba radhi kwa kuwapoteza Waislamu wenzetu wa Kisomali na tunatuma rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulio hilo."
Watu 90 walipoteza maisha katika mripuko wa mabomu uliotokea karibu na makutano ya barabara ya Afgoye mjini Mogadishu Disemba 28, hujuma ya kigaidi ambayo al-Shabaab ilikiri kuitekeleza.