Watu milioni 45 wakabiliwa na njaa ambayo haijawahi kushuhudiwa kusini mwa Afrika
(last modified Sat, 18 Jan 2020 04:58:51 GMT )
Jan 18, 2020 04:58 UTC
  • Watu milioni 45 wakabiliwa na njaa ambayo haijawahi kushuhudiwa kusini mwa Afrika

Watu zaidi ya milioni 45 wengi wakiwa wanawake na watoto katika nchi 16 za Kusini mwa Afrika wanakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula kufuatia kujirudia kwa hali ya ukame, kusambaa kwa mafuriko na kuyumba kwa uchumi.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP wakati hali ikizidi kuwa mbaya katika mataifa hayo dunia inapaswa kuchukua hatua ili kuokoa maisha na kuziwezesha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mkurugenzi wa WFP kanda ya Kusini mwa Afrika Lola Castro amesema “Janga la njaa liko katika kiwango ambacho hatujawahi kukishuhudia huko nyuma na ushahidi unaonyesha kwamba hali itakuwa mbaya zaidi." Amesema msimu wa kila mwaka wa vimbunga umeanza na eneo hilo haliwezi kumudu marudio ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na vimbunga visivyo vya kawaida mwaka jana.

Maafa ya kimbunga nchini Msumbuji

Aidha amesema kwamba kipaumbele kwa sasa ni mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa haraka.

WFP inapanga kutoa msaada kwa watu milioni 8.3 katika nchi nane walio katika hali mbaya ya dharura ya njaa ambazo ni Zimbabwe, Zambia, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Lesotho, Eswatini na Malawi.

Hadi kufikia sasa WFP imepata dola milioni 205 tu kati ya dola milioni 489 inazohitaji kuwasaidia watu hao na hivyo kulazimika kukopa ili kuhakikisha chakula kinawafikia wenye mahitaji.