Jeshi la Somalia lazima shambulizi la al-Shabaab karibu na Mogadishu
Vikosi vya jeshi la Somalia vimefanikiwa kuzima shambulizi la usiku wa kuamkia leo la kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
Duru za kijeshi zimearifu kuwa, wanachama wa kundi hilo jana usiku walivamia mji wa Afgoye katika eneo la Lower Shabelle yapata kilomita 30 kusini magharibi mwa Mogadishu, lakini wanajeshi wa serikali walikabiliana nao vikali na kuwarejesha nyuma.
Hata hivyo jeshi la Somalia halijaeleza iwapo kuna askari au mwanamgambo yeyote wa al-Shabaab aliyeuawa katika mapigano hayo ya jana usiku.
Bashir Mayow, mkazi wa mji wa Afgoye amesema milio ya risasi ilirindima masaa kadhaa usiku wa jana wakati wa makabiliano hayo na kusababisha hali ya taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Alkhamisi usiku, wanachama 16 wa al-Shabaab waliangamizwa baada ya kukabiliwa vikali na vikosi vya usalama vya Somalia katika eneo la Shabelle ya Kati.
Aidha mapema mwezi huu, wanamgambo wasiopungua 33 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waliuawa katika operesheni mbili tofauti za jeshi kusini magharibi mwa Somalia.