Wacomoro washiriki uchaguzi wa Bunge uliosusiwa na vyama vya upinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58618-wacomoro_washiriki_uchaguzi_wa_bunge_uliosusiwa_na_vyama_vya_upinzani
Wananchi wa visiwa vya Comoro leo Jumapili wameshiriki katika awamu ya kwanza ya zoezi la uchaguzi wa Bunge uliosusiwa na vyama vya upinzani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 19, 2020 14:21 UTC
  • Rais Azali Assoumani
    Rais Azali Assoumani

Wananchi wa visiwa vya Comoro leo Jumapili wameshiriki katika awamu ya kwanza ya zoezi la uchaguzi wa Bunge uliosusiwa na vyama vya upinzani.

Habari zinasema zoezi hilo limeanza kwa kuchelewa katika mji mkuu wa Comoro, Moroni kutokana na hali mbaya ya hewa.  

Vyama vya upinzani vimetangaza kuwa vimesusia uchaguzi huo wa Bunge lenye viti 24 baada ya kutopata dhamana kwamba utakuwa huru, wa wazi na wa kidemokrasia.

Rais Azali Assoumani wa visiwa vya Comoro alishinda uchaguzi wa Rais kwa mara ya pili mfululizo kwenye uchaguzi wa Machi mwaka jana ambao wachambuzi wa mambo wanasema uligumbikwa na wizi na uchakachuaji wa kura.

Uchaguzi wa Bunge la Comoro umefanyika leo Jumapili

Assoumani ambaye amekanusha madai hayo alikuwa amevitaka vyama vya upinzani kutupilia mbali mgomo wao na kushiriki katika zoezi hilo la leo kwa ajili ya kujenga nchi.

Kambi ya upinzani ilitoa masharti kadhaa kwa ajili ya kushiriki katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuruhusiwa Wacomoro wanaoishi nje ya nchi wanaokadiriwa kuwa laki tatu, kushiriki katika uchaguzi huo. Ombi hilo limekataliwa na serikali ya Rais Azali Assoumani.