Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Libya wakutana Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58689-mawaziri_wa_mambo_ya_nje_wa_nchi_zinazopakana_na_libya_wakutana_algeria
Algeria leo itakuwa mwenyeji wa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Libya kitakachojadili mgogoro unaoendelea nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 23, 2020 04:11 UTC
  • Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Libya wakutana Algeria

Algeria leo itakuwa mwenyeji wa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Libya kitakachojadili mgogoro unaoendelea nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema, baada ya takribani wiki moja tangu ulipofanyika mkutano wa Berlin, Ujerumani uliolenga kubuni njia ya kutekeleza usitishaji vita nchini Libya, mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Tunisia, Chad, Mali na Niger leo watakuwa na kikao cha pamoja kitakachofanyika mjini Algiers kujadili mgogoro wa nchi hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas, naye pia ataelekea Algeria leo kwa mazungumzo.

Mkutano wa Berlin wa kujadili mgogoro wa Libya

Algeria, ambayo ina mpaka wa pamoja na Libya wenye urefu wa kilomita elfu moja inatazamiwa kupendekeza katika kikao hicho njia za kutafuta muafaka utakaowezesha kufikiwa makubaliano ya amani nchini humo. 

Serikali ya Algiers ina mawasiliano mazuri na pande zote hasimu nchini Libya; na katika wiki za karibuni, viongozi kadhaa wakiwemo mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Kiarabu na za Ulaya pamoja Uturuki wameelekea nchini Algeria kwa mazungumzo ya kujadili mgogoro wa Libya.

Algeria, ambayo kwa muda wa karibu mwaka mmoja imekuwa ikikabiliwa na matatizo yake ya kisiasa ya ndani inahofia vitisho vipya vya kiusalama hasa vya makundi yanayobeba silaha yaliyoko ndani ya ardhi ya Libya vya kuvamia nchi hiyo na kushambulia vituo vyake vya mafuta na gesi.../