Ankara: Uturuki haitatuma askari wala silaha nchini Libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema kwamba kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa katika mkutano wa Berlin nchini Ujerumani, Uturuki haitatuma tena askari wala silaha huko Libya.
Akibainisha suala hilo siku ya Jumatano, Mevlut Cavusoglu ameashiria kubadilishwa msimamo wa awali wa Uturuki kuhusiana na jambo hilo na kumtaka pia Khalifa Haftar, kamanda wa askari wanaojiita 'Jeshi la Taifa la Libya' aheshimu na kufungamana na juhudi za kutatua kisiasa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiafrika kwa ajili ya kurejesha utulivu nchini humo. Mevlut Cavusoglu ameyasema hayo katika hali ambayo awali Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alikuwa ametangaza kwamba nchi hiyo iko tayari kutuma askari na silaha nchini Libya kwa lengo la kuisaidia serikali inayotambulika rasmi kimataifa kukabiliana na waasi wanaoongozwa na Haftar.
Mkutano wa Berlin ulifanyika siku ya Jumapili ambapo wawakilishi wa nchi 12 na wa mashiriki manne muhimu ya kimataifa na kieneo walishiriki na kuamua kutotoa msaada wowote kwa pande zinazozozana nchini Libya.
Mapigano ya ndani Libya yalianza baada ya Khalifa Haftar ambaye kwa miaka mingi amekuwa akiungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Saudi Arabia, Misri, Imarati na nchi nyingine za Magharibi kuanzisha uasi mashariki mwa nchi, mapigano ambayo yalishika kasi hivi karibuni kufuatia uamuzi wa kamanda huyo muasi kuanzisha mashambulizi ya kutaka kuuteka mji mkuu wa Libya Tripoli mnamo mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2019, hatua ambayo ililaaniwa vikali na jamii ya kimataifa. Pamoja na hayo haionekani kuwa matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Uturuki yametokana na nia yao ya kubadilisha msimamo, bali yametolewa ikiwa ni katika juhudi zao za kujaribu kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi yao. Jambo hilo lilionekana wazi baada ya kukamilika kwa kikao cha Berlin ambacho kilisisitiza juu ya umuhimu wa kupunguzwa mgogoro wa Libya.
Nukta hii pia inapasa kuashiriwa kwamba Uturuki imejiainishia maslahi ya msingi na ya muda mrefu nchini Libya. Moja ya maslahi hayo ni mkataba wa masuala ya baharini uliotiwa saini baina ya serikali ya Ankara na Tripoli mwezi uliopita. Wakati huohuo, Uturuki inajaribu kuimarisha mashindano yake na Saudi na Imarati nchini Libya, mashindano ambayo ilishindwa huko nyuma na nchi mbili hizo za Kiarabu huko Misri.
Mienendo ya Uturuki katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita inabainisha wazi kuwa imekuwa ikijaribu kupunguza mashinikizo ya jamii ya kimataifa kuhusiana na hatua zake za kutiliwa shaka nchini Libya. Ni sawa kabisa na kama ilivyofanya nchini Syria ambapo ilitumia ndege za kijeshi kutuma nchini humo makundi ya kigaidi kwenda kupigana dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa nchi hiyo. Nchi hiyo imebadilisha mbinu hiyo na sasa inatuma magaidi hao katika nchi hiyo jirani kwa kutumia ndege za abiria wa kawaida.
Katika upande wa pili na kama alivyokiri Rais Erdoğan mwenyewe, shirika la ujasusi la Uturuki lina nafasi muhimu katika matukio yanayojiri huko Libya. Sehemu ya shughuli za shirika hilo ni kuandaa ripoti za siri, ndege zisizo na rubani, magari ya kijeshi na pia kutuma makundi tofauti ya vibaraka wake nchini Libya.
Pamoja na hayo inaonekana kuwa tokea sasa Uturuki itakuwa ikifuatilia kwa karibu na kuwa na nafasi ya siri zaidi katika matukio ya Libya. Suala hilo linapata umuhimu maradufu kwa kutilia maanani kwamba huo ni mgogoro wa kwanza wa aina yake ambao unaendelea mbali na mpaka wa Uturuki na ambao nchi hiyo ina nafasi ya moja kwa moja ndani yake.