Kuendelea mgogoro nchini Libya, Haftar azidi kupiga ngoma ya vita
Vita nchini Libya vimeanza upya licha ya kuweko juhudi kubwa za kimataifa za kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Juhudi mbalimbali za kuyakusanya pamoja makundi hasimu ya Libya zilizofanyika katika nchi mbalimbali kama Moscow Russia, Berlin Ujerumani na Algiers nchini Algeria zimeshindwa kutuliza hali ya mambo nchini humo.
Mkwamishaji mkuu wa jitihada zote hizo anaonekana ni jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye amesema hadharani kuwa, mgogoro wa Libya hauna utatuzi wa kisiasa bali vita ndivyo vitakavyoamua. Jenerali huyo muasi ambaye anaungwa mkono kikamilifu ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na baadhi ya nchi za Magharibi, mwezi Aprili mwaka jana alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na jamii ya kimataifa.
Kitendo cha Jenerali Haftar cha kukoleza moto wa vita nchini Libya kimepelekea askari wa ndani na nje ya nchi hiyo wapige kambi za mapambano yasiyo ya moja kwa moja baina yao. Imarati, Saudia na Misri ziko katika kambi inayomsaidia kwa kila hali jenerali huyo muasi. Upande wa pili, yaani kambi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj inaungwa mkono waziwazi na Uturuki ambayo imefikia hadi kutuma wanajeshi wake nchini Libya kwenda kuisaidia serikali hiyo. Hali hiyo imezifanya nchi za kieneo na kimataifa pamoja na Umoja wa Mataifa kulipa umuhimu mkubwa zaidi suala la kutatuliwa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo. Juhudi kubwa zinazofanywa na jamii ya kimataifa hivi sasa ni kuhakikisha makubaliano ya kusimamisha vita yanafikiwa na kuheshimiwa na pande zote. Hata hivyo juhudi zote hizo zinakwamishwa na uasi wa Jenerali Khalifa Haftar ambaye amekuwa akianzisha mashambulizi mapya dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, mara tu ya kumalizika kila mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo. Khalifa Haftar alitoka kwenye mazungumzo ya Moscow kabla hayajamalizika, na alipoalikwa kushiriki mkutano wa Berlin, Ujerumani, alikataa kwenda. Baada ya mikutano ya Moscow na Berlin, kulifanyika pia kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazopakana na Libya huko Algiers, mji mkuu wa Algeria, lakini nacho kimeshindwa kumkinaisha Haftar kukubali kutumia njia za kisiasa kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Siku kadhaa zimepita sasa tangu kufanyika vikao hivyo, lakini Khalifa Haftar angali anaendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Tripoli na baya zaidi ni kwamba jenerali huyo muasi sasa amepanua wigo wa mashambulizi yake kwa kulenga pia uchumi wa Libya. Hivi sasa kiongozi huyo wa wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" ameamua kupiga marufuku bandari za nchi hiyo kusafirisha nje mafuta. Jambo hilo kwa kweli ni pigo kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo huku wataalamu wa mambo wakisisitiza kwamba, kitendo hicho ni sawa na kulipigilia msumari wa mwisho jeneza la maisha ya wananchi wa Libya.
Hatua hiyo ni hatari kwa uchumi wa Libya kiasi kwamba Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo ametahadharisha kuwa, huo ni msumari wa mwisho katika jeneza la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Gavana huyo wa Benki Kuu ya Libya, Sadiq al Kabir aidha amesema, kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuzuia kutokea maafa nchini Libya kwani kuzuiwa mafuta ya Libya yasitoke kwenye bandari za nchi hiyo ni sawa na msumari wa mwisho wa jeneza la nchi hiyo. Amesema, kwa vile uuzaji nje mafuta unadhamini asilimia 93 hadi 95 ya pato la Libya na hugharamia hadi asilimia 70 ya mahitaji ya nchi hiyo, kupiga mafuruku kusafirishwa nje mafuta ya nchi hiyo ni pigo kubwa kwa uwepo wa nchi hiyo.
Cha kusikitisha zaidi ni kuona kuwa waungaji mkono wa pande hasimu huko Libya nao hawaheshimu makubaliano ya kusimamisha vita wala marukufu ya kupeleka silaha nchini humo. Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Libya imesema kuwa, katika kipindi cha siku 10 zilizopita, shehena kadhaa za ndege zimetua katika viwanja vya ndege vya mashariki na magharibi mwa Libya zikiwa zimejaa silaha za kisasa, magari ya deraya, washauri wa kijeshi wa wapiganaji mamluki kwa ajili ya kuzisaidia pande hasimu nchini humo.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, licha ya kwamba waungaji mkono wa pande hasimu nchini Libya wanashiriki kwenye mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo lakini wenyewe hawana imani na utatuzi wa kisiasa.