Ufaransa yamwalika Haftar, kinara wa uasi Libya
Serikali ya Ufaransa imemualika mbabe wa kivita nchini Libya Jenerali Haftar ambaye ametenda jinai katika mkakati wake wa kuiondoa madarakani serikali ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ofisi ya Haftar Benghazi, Haftar alikutana na kuzunguza na mkurugenzi anayehusika na kitengo cha masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Afrika Kaskazini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa Christophe Farno.
Christophe Farno amemkabidhi mualiko Jenerali Haftar mualiko kutoka kwa rais Emmanuel Macron,wa kwenda nchini Ufaransa.
Hayo yanajiri wakati ambao msemaji wa vikosi vya wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) vinavyoongozwa na Khalifa Haftar amesema, vikosi hivyo havitaruhusu ndege za Umoja wa Mataifa kutumia uwanja pekee wa ndege unaofanya kazi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Ahmed Mismari amewaeleza waandishi wa habari katika mji wa Benghazi huko mashariki mwa Libya kuwa, ndege za Umoja wa Mataifa zitapaswa kutumia viwanja vingine vya ndege kikiwemo cha Misrata, kwa sababu LNA haiwezi kuhakikisha usalama wa ndege zinazoelekea uwanja wa ndege wa Mitiga ulioko mjini Tripoli kutokana na Uturuki kuutumia uwanja huo kama kituo chake cha kijeshi.
Tangu mwezi Aprili mwaka jana, kundi la LNA, ambalo linaungwa mkono na Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu limekuwa likijaribu kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli lakini hujuma na mashambulio yake yameshindwa kuvunja ngome za vikosi vya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa (GNA) inayoongozwa na Fayez al-Sarraj na ambayo ndiyo inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.