Wanamgambo wa ADF waua raia wengine 15 Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59250-wanamgambo_wa_adf_waua_raia_wengine_15_kongo_dr
Watu wasiopungua 15 wameuawa huku wengine zaidi ya 10 wakitekwa nyara katika shambulio linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Uganda wa ADF huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2020 04:39 UTC
  • Wanamgambo wa ADF waua raia wengine 15 Kongo DR

Watu wasiopungua 15 wameuawa huku wengine zaidi ya 10 wakitekwa nyara katika shambulio linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Uganda wa ADF huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, raia hao wameuawa kwa kuchomwa visu na kupigwa mapanga usiku wa kuamkia jana Jumanne huko Alungupa, eneo la  Rwenzori, wilayani Beni.

Naibu msemaji wa jeshi la Kongo FARDC, Brigedia Jenerali Sylvain Ekenge, amethibitisha habari hiyo ingawaje amesema idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo ni saba, huku akisisitiza kuwa jeshi linawasaka kwa udi na uvumba waliohusika na jina hiyo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu 30 waliuawa katika shambulizi jingine la wanamgambo hao wa ADF walioshambulia vijiji vinne katika mji wa Beni wa mashariki mwa nchi.

Wanajeshi wa DRC katika doria

Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi. 

Karibu raia 200 waliuawa katika mikoa miwili ya mashariki mwa DRC katika makabiliano baina ya maafisa usalama na magenge ya wanamgambo likiwemo kundi la waasi la ADF la Uganda ndani ya siku 31 za mwezi Disemba mwaka uliopita 2019.