Waziri Mkuu wa Libya: Haftar ni mtenda jinai za kivita
Fayez al Serraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amelaani kushambuliwa maeneo ya raia na viwanja vya ndege nchini humo kunakofanywa na wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.
Akihutubia jana katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Fayez al Serraj amemtaja Haftar kuwa mtenda jinai za kivita.
Amesema watoto wa Libya wamepoteza haki yao ya kwenda shule kutokana na mashambulizi na kufungwa shule kunakosababishwa na Haftar na wale wote wanaomfadhili kifedha na kumpatia silaha. Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ameongeza kuwa wale wote wanaomuunga mkono mtenda jinai Khalifa Haftar wanapasa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Ameongeza kuwa serikali yake inayotambuliwa kimataifa mara zote imeonyesha utayarifu wake wa kwenda mbele katika njia ya amani na uthabiti.
Wakati huo huo mazungumzo ya kisiasa kati ya pande mbili zinazozozana huko Libya chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa yamepangwa kufanyika kesho Jumatano huko Geneva Uswisi. Itakumbukwa kuwa Siku chache zilizopita, Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Baraza la Uongozi na Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa alisitisha ushiriki wake katika mazungumzo huko Geneva akilalamikia mashambulio ya mizinga ya Khalifa Haftar dhidi ya mji mkuu Tripoli. Hivi sasa Haftar sambamba na kulaani hatua hiyo ya Fayez al-Sarraj amesema kuwa, sharti lake la kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita ni kuondoka Uturuki katika ardhi ya Libya.