Marekani na al-Shabaab zalaumiana kuhusu mauaji ya raia Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59480-marekani_na_al_shabaab_zalaumiana_kuhusu_mauaji_ya_raia_somalia
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limesema zaidi ya asilimia 80 ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani nchini Somalia yanalenga raia wasio na hatia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2020 04:44 UTC
  • Marekani na al-Shabaab zalaumiana kuhusu mauaji ya raia Somalia

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limesema zaidi ya asilimia 80 ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani nchini Somalia yanalenga raia wasio na hatia.

Katika taarifa ya jana Jumamosi, genge hilo lenye mfungamano na mtanadao wa kigaidi wa al-Qaeda limesema Marekani imekuwa ikiua raia kwenye mashambulizi hayo kwa kutumia ndege zake zisizo na rubani (drone), na kisha kuhalalisha kwa kusema kuwa imelenga ngome za magaidi kwenye hujuma hizo.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa al-Shabaab, Ali Muhamud Rageh 'Ali Dhere' imedai kuwa, asilimia 82.7 ya mashambulizi ya drone ya Marekani ndani ya miezi 34 nchini Somalia ililenga raia wasio na hatia. Imeongeza kuwa, asilimia 37 ya waliolengwa kwenye hujuma hizo ni wakulima, asilimia 24.3 wanawake, na asilimia 21.4 watoto wadogo.

Hata hivyo Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM imetoa taarifa na kudai kuwa watu waliouawa kwenye hujuma zake za anga walikuwa watu wanachama wa magenge yenye misimamo ya kufurutu ada. AFRICOM inadai kuwa ilitekeleza mashambulizi 63 ya drone mwaka jana, na kuua makumi ya magaidi wa al-Shabaab.

Raia wa Somalia ni wahanga wa hujuma za al-Shabaab na mashambulio ya drone ya Marekani

Hii ni katika hali ambayo, Oktoba mwaka jana, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema jeshi la Marekani limeua raia wasio na hatia katika moja ya mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Aidha kabla ya hapo, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.