Mar 09, 2020 04:34 UTC
  • Waasi waua wanajeshi watano na raia wanne nchini Cameroon

Waasi wamemeshambulia kituo cha polisi kilichoko wilayani Galim magharibi mwa Cameroon na kuua wanajeshi watano na raia wanne.

Taarifa zinasema hujuma hiyo ya usiku wa kuamkia Jumapili ilitekelezwa na waasi hao takriban 20 wakiwa wamepanda pikipiki katika mkoa huo ambao wakaazi wake wengi wanazungumza Kifaransa. Imedaiwa kuwa shambulizi hilo limetekelezwa na waasi kutoka eneo linalozungumza Kiingereza nchini humo ambao wanapigana kujitenga.

Gavana wa eneo la magharibi mwa Cameroon Awa Fonka Augustine amesema wanawasaka waasi waliotekeleza hujuma hiyo.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 3,000 wameuawa nchini Cameroon tokea mwaka 2017 na wengine 530,000 kukimbia makazi yao kufuatia kuanza uasi katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. Wazungumzaji hao wa Kiingereza wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wameanzisha uasi wakitaka kujitenga.

Tags