Kuendelea mashauriano kwa ajili ya kurejesha hali ya uthabiti Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59671-kuendelea_mashauriano_kwa_ajili_ya_kurejesha_hali_ya_uthabiti_libya
Katika hali ambayo vita vinaendelea huko Libya; Khalifa Haftar kamanda wa wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya ameainisha masharti kwa ajili ya kutekeleza usitishaji vita huko Libya wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika ikulu ya Elysee.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 11, 2020 07:08 UTC
  • Kuendelea mashauriano kwa ajili ya kurejesha hali ya uthabiti Libya

Katika hali ambayo vita vinaendelea huko Libya; Khalifa Haftar kamanda wa wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya ameainisha masharti kwa ajili ya kutekeleza usitishaji vita huko Libya wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika ikulu ya Elysee.

Haftar ameeleza kuwa yupo tayari kusaini makubaliano ya kusitisha vita iwapo vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa vya Libya vitaheshimu pia makubaliano hayo. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Jenerali Haftar katika ikulu ya Elysee Paris 

Safari ya Haftar nchini Ufaransa inafanyika katika hali ambayo kufuatia kushtadi vita huko Libya katika miezi ya karibuni kumefanyika jitihada mbalimbali za kimataifa kwa lengo la kuivusha nchi hiyo katika hali ya mgogoro wa hivi sasa na kufanikisha usitishaji vita nchini humo. Haftar ambaye anadhibiti maeneo ya mashariki mwa Libya anaungwa mkono kwa hali na mali na baadhi ya pande za kieneo na kimataifa zikiwemo Misri, Saudi Arabia na Imarati. Khalifa Haftar alianzisha duru mpya ya mashambulizi tangu mwanzoni mwa mwaka uliopita wa 2019 kwa lengo la kuuteka mji mkuu Tripoli unaodhibiti na serikali ya umoja wa kitaifa na kwa lengo la kuunda serikali kuu huko Libya. Hali hiyo ya mambo imeshadidisha mgogoro nchini humo na kupelekea nchi ajinabi ziingilie kijeshi huko Libya. Hali ya mchafukoge imewapelekea wengi kutahadharisha juu ya uwezekano wa kubadilika vita vya Libya na kuwa vita vya kieneo. 

Ghassan Salame Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametahadharisha kuhusu kubadilika mapigano huko Libya na kuwa vita vya kieneo na kueleza kuwa: Libya inahitaji kuona uingiliaji wote wa nchi ajinabi ukisitishwa nchini humo. 

Ghassan Salame, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya

Pamoja na hayo vita vingali vinaendelea huko Libya licha ya kuongezeka jitihada za kimataifa za kusuluhisha na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa sasa nchini humo kuhusu suala la kufanyika mazungumzo ikiwemo kufanyika mkutano huko Berlin Ujerumani. Aidha  zjitihada zinaendelea kufanywa ili kutekelezwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya ili kukomeshwa hali ya mgogoro nchini humo. Licha ya jitihada zote hizi, wanamgambo hao wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar siku kadhaa zilizopita walitekeleza mashambulizi dhidi ya miundo mbinu ukiwemo uwanja wa ndege wa Tripoli. Si hayo tu wanamgambo hao walizishambulai pia nyumba za raia katika eneo moja karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mitiga pia na kusababisha vifo na kujeruhi watu kadhaa.   

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetangaza kuwa: Uingizaji silaha na mada za milipuko huko Libya umeongezeka katika mwaka huu wa 2020, zana za kijeshi zinazidi kumiminika nchini humo na maelfu ya familia za Kilibya zimelazimika kuwa wakimbizi kutokana na kushtadi mapigano. Wakati huo huo mapigano hayo yamesababisha hasara na maafa chungu nzima kwa miundo mbinu ya nchi kiasi kwamba aghalabu ya wananchi wa Libya wanataabika pakubwa kupata mahitaji yao ya dharura na bidhaa za msingi.    

Nchi ajinabi zimeshadidisha uingiliaji wao nchini humo licha ya hali hii ya mambo. Ufaransa ni moja ya nchi hizo zinazotekeleza uingiliaji wao katika masuala ya kisiasa huko Libya. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika miaka kadhaa ya karibuni amekutana na kufanya mazungumzo mara kadhaa na Khalifa Haftar na pia Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya; na licha ya kufanya juhudi za kuonyesha kutoegemea upande wowote viongozi wa Paris katika mgogoro wa Libya lakini nchi hiyo inamuunga mkono Haftar ili kulinda maslahi ya Paris katika nchi hiyo ya Kiafrika. Hivi sasa pia Ufaransa inafanya kila iwezalo ili kubadili hali ya kisaisa ya Libya kwa maslahi yake. Aidha mbali na utajiri na maliasili ya mafuta ilionao Libya ambao siku zote umekuwa ukizingatiwa na kukodolewa macho pakubwa na viongozi wa Paris ambapo baadhi ya makampuni ya mafuta ya Ufaransa yangali yanaendesha shughuli zake huko Libya; kwa mtazamo wa Paris nchi hiyo inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kudhibiti wimbi la wahajiri haramu kuelekea Ulaya na kukabiliana na makundi ya kigaidi kutokana na nafasi yake kwa upande wa  jiopolitiki na kuwa kwake karibu na Ulaya. Hasa ikizingatiwa kuwa Libya ni miongoni mwa nchi muhimu za kaskazini mwa Afrika na inayohesabiwa kama lango la kuingia Afrika. Katika mazungumzo yake na Macron; Haftar amesisitiza kuwa ataheshimu makubaliano ya usitishaji vita kwa sharti kwamba upande wa pili yaani serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya pia uheshimu makubaliano hayo. Hata kama mashauriano ya kisiasa yangali yanaendelea lakini inaonekana kuwa suala la maslahi ni kikwazo kikuu katika njia ya kurejeshwa amani na uthabiti wa kisiasa nchini humo.