Serikali ya Guinea yasema ugonjwa wa corona hautazuia uchaguzi
Serikali ya Guinea-Conakry imesisitiza kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge na kura ya maoni ya katiba pamoja na kuwa wapinzani wanataka uchaguzi usitishwe kutokana na hofu ya kuenea ugonjwa wa COVID-19 au corona.
Aidha wapinzani wanautazama uchaguzi huo ambao utafanyika kesho Jumapili kuwa mbinu za rais Alpha Condé ambaye anataka kubadilisha katiba ili aweze kuwania muhula wa tatu kinyume cha sheria ya sasa.
Ingawa katiba mpya ambayo inatazamiwa kuidhinishwa katika kura ya maoni ina kipengee cha mihula miwili ya rais ambayo sasa imeongezwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba, lakini rais Conde amesema mihula yake iliyopita haipaswi kuzingatiwa na hivyo anaweza kugombea mihula mingine miwili.
Serikali imesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa kuahirishwa matukio hayo muhimu kwa nchi na maandalizi yanaendelea vizuri licha ya janga la Covid-19 ambalo Guinea imethibitisha kesi mbili za maambukizi ya kirusi cha ugonjwa huo.

Hata hivyo kiongozi mkuu wa upinzani, Cellou Dalein Diallo, amesema kuwa uamuzi wa serikali wa kuandaa uchaguzi huo hauendani "na hali ya sasa ya kiafya.
"Ni kutowajibika, ni kosa la jinai. Serikali haiwajibiki, haina hata wasiwasi na maisha na afya ya raia wa Guinea. Alpha Condé anataka tu kuwania muhula wa tatu. Sisi, tunawaambia watu: msendi kupiga kura kwa kuhatarisha afya yenu, ili msihusiki katika jaribio hilo la mapinduzi ya katiba ambayo Alpha Condé anataka kufanya. "
Waziri wa Habari wa nchi hiyo, Amara Somparé amesema kwa sasa, janga la COVID-19 limedhibitiwa.