Ugonjwa wa corona wazidi kuenea Afrika, 800 waambukizwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59869-ugonjwa_wa_corona_wazidi_kuenea_afrika_800_waambukizwa
Kesi za maambukizi ya ugonjwa wa corona au COVID-19 barani Afrika zimepita 800 hadi kufikkia Ijumaa huku nchi mbalimbali zikiiimarisha hatua za kukabiliana na ugonjwa huo unaoenea kwa kasi kote duniani.
(last modified 2026-01-01T09:10:44+00:00 )
Mar 21, 2020 01:35 UTC
  • Ugonjwa wa corona wazidi kuenea Afrika, 800 waambukizwa

Kesi za maambukizi ya ugonjwa wa corona au COVID-19 barani Afrika zimepita 800 hadi kufikkia Ijumaa huku nchi mbalimbali zikiiimarisha hatua za kukabiliana na ugonjwa huo unaoenea kwa kasi kote duniani.

Kwa mara ya kwanza, Chad, Niger na Cape Verde zimeripoti kesi za maambukizi ya kirusi cha corona. Huko mashariki mwa Afrika, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa kirusi hicho ikiongezeka katika nchi za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa taarifa aghlabu ya wagonjwa wa COVID-19 barani Afrika wametokea Ulaya na Marekani, na ili kuzuia ueneaji wa janga hili, nchi mbalimbali barani humo zimesimamisha safari za ndege kutoka nchi zilizokumbwa zaidi na janga hilo haswa nchi za Ulaya.

Hatua nyingine zisizo za kawaida pia zimechukuliwa na nchi za bara hilo. Afrika Kusini imetangaza kuwa, watu wanaoeneza kirusi cha corona kwa makusudi watashtakiwa kwa kosa la mauaji. Tanzania nayo imepiga marufuku kutembelea wafungwa ili kuzuia kuenea kirusi hicho gerezani. Serikali ya Zimbabwe imepanga kutenga dola milioni 26.4 za Kimarekani katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Nayo serikali ya Afrika Kusini imesema inajiandaa kujenga uzio wa kilomita 40 katika mpaka wa nchi hiyo na Zimbabwe, kwa lengo la kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini humo, na pia kuzuia kuenea corona.