Jeshi la Somalia laua magaidi 12 wa al-Shabaab kusini mwa Somalia
Wanachama 12 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la Bay, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Mohamed Abdullahi, kamanda wa Kikosi cha 60 cha Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) ambaye ameongeza kuwa, wanachama wengine 10 wa genge hilo wamejeruhiwa.
Amesema wanajeshi wa Somalia walijibu mapigo na kuwashambulia magaidi hao, baada ya kushambulia kambi ya jeshi la serikali katika eneo la Bay, kusini mwa nchi ambapo walifurushwa na wengine wakakimbilia msituni.
Haya yanajiri siku tatu baada ya vikosi vya serikali vikishirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (Amisom) kuua wanachama wengine sita wa al-Shabaab katika operesheni dhidi ya maficho ya magaidi hao katika vijiji vya eneo la Lower Juba, kusini mwa nchi.
Aidha wiki mbili zilizopita, Jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa Amisom lilifanikiwa kuukomboa mji wa kistrataji wa Janale ulioko kwenye eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia, toka mikononi mwa al-Shabaab.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.