May 17, 2020 08:00 UTC
  • Wanachama tisa wa Boko Haram wauawa katika mapigano na jeshi la Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa limewaua wanamgambo tisa wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika mapigano yaliyotokea kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi la Nigeria limeeleza katika taarifa kuwa, wanamgambo wa Boko Haram walifanya shambulio dhidi ya kambi moja ya jeshi iliyoko katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya shambulio hilo yalizuka mapigano kati ya wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi na vikosi vya jeshi ambapo wanamgambo tisa wa Boko Haram waliuawa na magari mawili na zana kadhaa za kundi hilo ziliteketezwa.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, askari wawili wa jeshi la Nigeria pia waliuawa katika mapigano hayo.

Wanamgambo wa kundi la Boko Haram

Boko Haram ni kundi la kigaidi linalobeba silaha ambalo lilianzisha harakati zake nchini Nigeria Januari 2002.

Mashambulio na hujuma za kigaidi za kundi hilo, hasa kuanzia mwaka 2009 ndani ya Nigeria zilisababisha maelfu ya watu kuuawa na mamilioni kupoteza makazi yao.

Mnamo mwaka 2015, mbali na Boko Haram kutangaza kiapo cha utiifu kwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, lilipanua pia wigo wa mashambulio yake ya kigaidi nje ya mipaka ya Nigeria katika nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon.../

Tags