Tanzania yafungua anga na kuruhusu ndege kuendelea kuingia na kutoka nchi hiyo
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza rasmi kufungua anga yake na kuruhusu ndege zote kuendelea kutua au kupita katika anga ya nchi hiyo baada ya kufungwa kuanzia tarehe 7 Mei mwaka huu katika jitihada za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.
Itakumbukwa kuwa tarehe 7 Mei mwaka huu serikali ya Tanzania ilitangaza kufunga viwanja vyake vya ndege na kuzuia dege kutoka nje ya nchi kutua nchini humo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kwamba, kuanzia leo serikali imeondoa zuio hilo na kuruhusu ndege zote kuendelea kutua. "Baada ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa huo (Covid-19) hapa Tanzania kama ilivyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jana Mei 17, 2020, imebainika kuwa udhibiti wa ugonjwa huo umeendelea kuimarika. Wagonjwa wamekuwa wakipungua katika vituo mbalimbali vya afya nchini hivyo Serikali inatangaza kufungua anga lake rasmi kuanzia leo tarehe 18, Mei, 2020." Amesema Mhandisi Isack Kamwelwe.
Aidha amebainisha kwamba kuanzia sasa ndege zote za kibiashara, misaada, kidiplomasia , dharura na ndege maalumu zinaruhusiwa kuruka, kutua, na kupita juu ya anga ya Tanzania kama ilivyokuwa hapo awali. Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, amebainisha kuwa taratibu za kiafya zilizowekwa na shirika la afya Duniani (WHO) pamoja na Wizara ya Afya zitaendelea kuzingatiwa wakati wote. Kwa mujibu wa Mhandisi Isack Kamwelwe, serikali itahakikisha abiria wote wanaoingia na kutoka nchi hiyo wakipimwa joto na endapo watahisiwa kuwa na viashiria vya virus vya Corona watawekwa sehemu maalumu kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Kadhalika ameitaka mamlaka ya usafiri wa anga nchini Tanzania (TCAA) kuliarifu Shirika la anga la kimataifa kuhusu maamuzi haya na kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa bilakuwepo vikwazo vyovyote. Jumapili ya jana Rais John Pombe Magufuli alisema kuwa serikali ya Tanzania haiwezi kutekeleza hatua za kuwazuia watu kutoka nje ya nchi kwani huo ni ugonjwa mkubwa zaidi kuliko hata Corona yenyewe.