May 21, 2020 07:50 UTC
  • Watu 287 wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini

Mamia ya watu wameuawa katika mapigano ya kikabila katika jimbo la Jonglei, mashariki mwa Sudan Kusini.

Maafisa wa serikali katika eneo hilo wameiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar jana Jumatano kuwa, kwa akali watu 287 akiwemo mfanyakazi wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka wameuawa katika mapigano hayo.

Kwa mujibu wa serikali, watu 300 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya Jumamosi baina ya makabila ya Murle na Lou Nuer katika jimbo hilo la mashariki mwa nchi.

Mbali na afisa mmoja wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka kuuawa, wahudumu wengine wawili wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) wameuawa kwenye ghasia hizo za kikabila.

Wanavijiji wakiyahama makazi yao wakikimbia mapigano

Kamishna wa kaunti ya Uror, John Dak Gatluak amesema mapigano hayo yalianza baada ya kundi la kabila la Murle kushambulia vijiji sita vya watu wa kabila la Lou Nuer siku ya Jumamosi.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika yamepelekea watu zaidi ya 380,000 kuuawa, mbali na mamlioni kufurushwa kwenye makazi yao na kuwa wakimbizi katika kipindi cha miaka sita. 

 

Tags