Ajali ya boti yaua watu Ziwa Tanganyika nchini Tanzania
Watu wasiopungua tisa wamefariki na wengine 51 wamejeruhiwa baada ya meli kuzama katika Ziwa la Tanganyika nchini Tanzania.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma Martin Otieno, amesema ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri siku ya Alhamisi wakati meli hiyo ikisafiri kutoka Sibwesa kwenda Ikola mkoani Katavi.
Meli hiyo iliyozama iliyojulikana kama MV Nzaimana ilikuwa na abiria 60 na mizigo ilipinduka baada ya kukumbwa na dhoruba. Miili ya waliofariki imegunduliwa ikiwa ni wanawake saba na wanaume wawili.
Ajali za boti na meli hujiri mara kwa mara nchini Tanzania. Ajali ya hivi karibuni ilijiri Septemba 2018 wakati meli ilipozama katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania na kuua watu wasiopungua 200.