Ghasia na maandamano Ethiopia baada ya mwanaharakati kuuawa
Ghasia zimeibuka katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa baada ya muimbaji na mwanaharakati mashuhuri kupigwa risasi na kuuawa.
Haacaaluu Hundeessaa, aliuawa mjini Addis Ababa Jumatatu usiku na baada ya hapo ghasia zikaanza katika mji huo huku waandamanaji wakiwasha moto barabarani. Hundeessaa, 34, ambaye ni kutoka kabila la Oromo alikuwa mashuhuri kwa nyimbo zake za kimapinduzi na kutetea haki. Mkuu wa Polisi mjini Addis Ababa Geta Argaw amesema mwanaharakati huyo alikimbizwa hospitalini baada ya kupigwa risasi lakini alifariki kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata. Bado haijajulikani ni nani aliyehusika na mauaji hayo ambayo yamelaaniwa na maafisa wa serikali na raia ndani na nje ya nchi hiyo.
Wafuasi wake wanasema aliuawa kutokana na nyimbo zake ambazo zilikuwa zinawahimiza watu wa kabila la Oromo waamke kutetea haki zao na wapambane na ukandamizaji. Ingawa kabila la Oromo ndilo kubwa zaidi nchini Ethiopia lakini kwa muda mrefu Waoromo wamekuwa wakilalamika kuwa wanabaguliwa na kutengwa. Baba yake Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ni kutoka kabila la Oromo na mama yake ni kutoka kabila la Amhara.
Mauaji hayo yamezidisha taharuki za kisiasa katika nchi hiyo ambayo inaendeleza mchakato kuimarisha demokrasia. Taarifa zinasema mawasiliano ya intaneti yamekatwa katika nchi hiyo, ikiwa ni hatua ya kawaida ambayo huchukuliwa mara kwa mara wakati wa ghasia za kisiasa.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametuma salamu za rambi rambi na ametoa wito kwa wananchi watulie huku akisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu mauaji hayo.