Jul 05, 2020 14:23 UTC
  • Waziri Mkuu Sudan aahidi kutimiza matakwa ya Wasudan katika wiki mbili zijazo

Waziri Mkuu wa Sudan amesema kuwa amekutana na makundi mbalimbali ya kisiasa na kijamii katika siku chache zilizopita na kupokea miito inayomtaka asahihishe mwelekeo wa serikali yake na kutimiza malengo ya mapinduzi ya Wasudani yaliyomuondoa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Abdallah Hamdok amesema matakwa yote ya wanamapinduzi yalikuwa halali na kwamba atafanya jitihada kubwa za kuyatekeleza katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Amesema serikali yake inakabiliana na changamoto nyingi katika kipindi hiki cha mpito na kwamba Sudan inakabiliana pia na madola ya kigeni yanayofanya njama za kuteteresha usalama wake.

Wakati huo huo chama cha upinzani cha Kongresi ya Wananchi kilichoanzishwa na Dakta Hassan Turabi kimekosoa kamatakamata inayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi wa vyama na wanaharakati wa masuala ya siasa. Chama hicho kimesema kamatakamata hiyo inafanyika kinyume cha sheria na inakiuka haki za binadamu.

Vyombo vya usalama vya Sudan vimewatia nguvuni viongozi wa upinzani

Taarifa iliyotolewa na chama hicho imesema familia za baadhi ya wanasiasa za upinzani waliotiwa nguvuni zinasema kuwa, watu hao wamepotezwa na vyombo vya usalama na hawajulikani waliko.  

Vilevile kimezitaka jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu kuishinikiza serikali ya Khartoum ili iwaachie huru wafungwa wa kisiasa na wale waliowekwa mahabusu kutokana na rai na mitazamo yao.     

Tags