Burundi yabadili sera, yaanza upimaji COVID-19 mjini Bujumbura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62066-burundi_yabadili_sera_yaanza_upimaji_covid_19_mjini_bujumbura
Serikali ya Burundi imezindua operesheni ya upimaji mkubwa wa maambukizi ya COVID-19 katika mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo Bujumbura.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 08, 2020 02:55 UTC
  • Burundi yabadili sera, yaanza upimaji COVID-19 mjini Bujumbura

Serikali ya Burundi imezindua operesheni ya upimaji mkubwa wa maambukizi ya COVID-19 katika mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo Bujumbura.

Bw. Ndikumana pia amesema, operesheni hiyo imechagua mji wa Bujumbura kutokana na kuwa maambukizi mengi ya COVID-19 yametokea mjini humo.

Waziri huyo pia amesema serikali inapanga kuanza upimaji kwenye maeneo mengine kabla ya Ijumaa, wakianza na maeneo ya miji mikuu ya mikoa.

Tokea mwezi Machi, ni watu 3,000 pekee waliopimwa COVID-19 nchini Burundi na miongoni mwao watu 191 walipatikana na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa takwimu rasmi ni mtu mmoja tu aliyefariki huku asilimia 80 ya walioambukizwa wakiruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kupata matibabu hospitalini.

Mnamo Juni 30, Rais Evariste Ndayishimiye alisema COVID-19 ni adui mkubwa wa Warundi wote na kutangaza azma yake ya kukabiliana na ugonjwa huo. Aidha alitangaza kuwa bei ya sabuni itapunguzwa kwa asilimia 50 ili kuwawezesha wananchi kukabiliana na ugonjwa huo kwa kunawa mikono mara kwa mara. Hali kadhalika alisema serikali itapunguza bei ya maji katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo hasa miji mikubwa hadi pale ugonjwa wa COVID-19 utakapoangamizwa.