Jul 14, 2020 07:59 UTC
  • Askari 10 wa Nigeria wauawa katika mashambulizi ya kigaidi

Duru za kiusalama nchini Nigeria zimetangaza habari ya kuuawa wanajeshi kumi wa nchi hiyo katika mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi kaskazini mashariki mwa nchi.

Shirika la habari la AFP limenukuu duru za kiusalama zikithibitisha habari ya kutokea mashambulizi hayo mawili yaliyofanywa jana Jumatatu na magenge ya kigaidi, huko kaskazini mashariki mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, askari wanane waliuawa baada ya msafara wa magari yao kushambuliwa na genge la kigaidi lililojizatiti kwa silaha katika kijiji kimoja kilichoko umbali wa kilomita 40 kutoka mji wa Maiduguri, makao makuu ya mkoa wa Borno.

Kadhalika wanajeshi wawili wa Nigeria wameuawa katika shambulizi jingine tofauti la jana pia, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram

Haijabainika iwapo hujuma hizo za kigaidi zimefanywa na kundi la kigadi na ukufurishaji la Boko Haram, au magenge mengine ya kigaidi yenye mfungamano na kundi la Daesh (ISIS).

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha harakati zake za uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi eti utawala wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo hivi sasa limepanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon na kuua makumi ya maelfu ya watu.

 

Tags