Jul 15, 2020 02:37 UTC
  • ICC yaanza kusikiliza kesi ya gaidi mtenda jinai kutoka Mali

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai imeanza kusikiliza kesi ya gaidi raia wa Mali ambaye anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai ya kubomoa maziyara matakatifu katika mji wa kale wa nchi hiyo, Timbuktu.

Kwa mujibu wa taarifa siku ya Jumanne mahakama ya ICC ilianza kusikiliza kesi ya gaidi huyo mwenye umri wa miaka 42 aliyetambuliwa kwa jina la  Al-Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud.

Mpiganaji huo wa kundi la kigaidi linalojiita Ansar Din, linalofungamana na Al Qaeda alikuwa anafanya uhalifu wake huko Timbuktu katika miaka ya 2012 and 2013. Mbali na kukabiliwa na mashtaka ya kubomoa maziyara, gaidi huyo pia anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, ubakaji na utumwa wa ngono.

ICC imesema gaidi huyo alikuwa mkuu wa 'kitengo cha polisi' katika kundi hilo la Ansar Din lenye itikadi za Kiwahabi za ukufurushaji.

Mashtaka hayo yanahusu kipindi ambacho magaidi hao wa kundi la Ansar Din walipotumia vibaya mwamko wa kabila la Tuareg mwaka 2012 ambapo waliteka miji kadhaa ya eneo la Kaskazini mwa Mali.

Msikiti wa kale wa Timbukutu 

Mji wa Timbuktu ambao ni maarufu kwa turathi za Kiislamu duniani unajulikana kama 'Mji wa Mawalii 333' ambao walizikwa hapo katika zama za kunawiri Uislamu eneo hilo katika karne zilizopita.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeuweka mji wa Timbuktu katika orodha ya miji ya kale inayokabiliwa na tishio la kuangamia.

Tags