May 12, 2019 14:55 UTC
  • Mhubiri wa Kiwahhabi aliyesoma Saudia akamatwa Sri Lanka, ahusishwa na ugaidi

Wakuu wa Sri Lanka wamemkamata mhubiri wa Kiwahhabi aliyesoma nchini Saudi Arabia baada ya kushukiwa kuwa na mfungamano na magaidi waliotekeleza hujuma za kigaidi zilizoua mamia ya watu nchini humo mwezi jana.

Katika hujuma hizo, magaidi walilipua mabomu katika makanisa na mahoteli ya kifahari katika mji mkuu wa Sri Lanka, Colombo na miji mingine mnamo Aprili 21 na kuua watu wasiopungua 253.

Polisi nchini Sri Lanka wamebaini kuwa hujuma hizo za kigaidi ziliratibiwa na Zahran Hashim, kinara wa kundi la Kiwahhabi linalojiita Nations Thawahid Jaman (NTJ). Hashim mwenyewe alijilipua na kuangamia katika hoteli ya kifahari mjini Colombo katika siku ya milipuko hiyo.

Hali ilivyokuwa baada ya hujuma za kigaidi msikitini nchini Sri Lanka

Polisi ya Sri Lanka imetangaza kumkamata Mohamed Aliyar, mwenye umri wa miaka 60, ambaye ni muasisi wa kituo kimoja cha Kiwahhabi katika mji wa Kattankudy alikozaliwa Zahran  mashariki mwa nchi hiyo.  Maafisa wa usalama wamebaini kuwepo uhusiano wa karibu baina ya Aliyar na Zahran. Taarifa zinasema Aliyar aliasisi kituo chake hicho mwaka 1990 baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Imam Muhammad bin Saud mjini Riyadh, Saudi Arabia. Kukamtwa mhubiri huyo kunatazamiwa kuangazia nafasi ya Uwahhabi katika kueneza ugaidi eneo la kusini mwa Asia. Wakuu wa Sri Lanka wamesema wamechukua hatua za kuzuia kueneza misimamo mikali katika nchi hiyo huku wengi wakiwa na hofu ya kutokea hujuma dhidi ya Waislamu kufuatia ugaidi wa Mawahhabi.

 

Tags