Wapiganaji 18 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waangamizwa nchini Somalia
Kwa akali wapiganaji 18 wa kundi la kiigaidi la al-Shabab wameangamizwa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya wanamgambo hao katika mji wa Jilib.
Jeshi la Somalia limethibitisha kuwa, operesheni ya wanajeshi wake katika mji wa Jilib wa kusini mwa nchi hiyo imepelea wanamgambo 18 wa kundi la al-Shabab wakiwemo viongozi wao wawili kuuawa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni jeshi la Somalia likishirikiana na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM limefanikiwa kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo hao wa Kitakfiri.
Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu miaka 30 iliyopita na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab walianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo mwaka 2008.
Mwaka 2011 magaidi wa Al Shabab walifurushwa Mogadishu katika oparesheni ya pamoja ya Jeshi la Somalia na Askari wa Kulinda Amani wa Umoja wa Afrika lakini pamoja na hayo magaidi hao bado wanadhibiti maeneo mengi nchini Somalia.
Kundi hilo linapigwa vita na wasomi wa Kiislamu wanaosema linafuata itikadi zisizo sahihi za kundi la Kiwahabi linalofasiri isivyo mafundisho na sheria za Uislamu.
Kundi la kigaidi la Al Shabab, linalofungamana na mtandao wa Al Qaeda hutekeleza mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara nchini Somalia hali ambayo imeifanya nchi hiyo kukosa amani na usalama.