FAO: Kenya imechukua hatua muafaka kuangamiza nzige
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linasema Kenya imepiga hatua kubwa katika kudhibiti nzige wa jangwani ambao walivamia eneo la Afrika Mashariki mapema na kwingineko mwezi February na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.
Uvamizi huo wa nzige ulihatarisha maisha ya mamilioni ya watu na uhakika wa chakula baada ya mazao kuharibiwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya FAO iliyotolewa Jumanne mjini Roma Italia kati ya nchi 29 zilizokumbwa na nzige hao waharibufu 26 zimefanikiwa kuwadhibiti lakini tatu bado zinapambana zikiwemo Kenya, Somalia na Ethiopia.
Hata hivyo shirika hilo linatumai kwamba katika siku chache zijazo zitasalia nchi mbili na ndani ya wiki tatu kwani Kenya itajikomboa kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na mafanikio hayo Cyril Ferrand kiongozi wa FAO wa masuala ya mnepo katika eneo la Afrika Mashariki ameonya kwamba nchi hizo zisibweteke kwani tishio la kuzuka upya mzunguko mwingine wa nzige wa jangwani mwishoni mwa mwaka huu bado lipo.
Ferrand amesema Ethiopia ingali inakabiliwa na tishio la nzige hao wa jangwani.
Ameongeza kuwa miongoni mwa nchi zote 29 zilizokumbwa na nzige wa jangwani mwaka huu Kenya ndiyo iliyoathirika vibaya zaidi baada ya kutoshuhudia nzige kwa miaka 70 ikifuatiwa na Ethiopia, Somalia na Sudan Kusini.
Juhudi kubwa za FAO kwa kushirikiana na wizara husika za kilimo na chakula katika nchi zilizoathirika zimefanikisha kuokoa karibu ekari laki sita Afrika Mashariki na kuua nzige bilioni 400 hatua iliyozuia uharibifu mkubwa wa mazao.
Makadirio ya FAO ni kwamba kati ya Juni na Desemba mwaka huu kutakuwa na idadi kubwa ya watu wasio na uhakika wa chakula Afrika Mashariki kutokana na nzige wa jangwani pekee na ukiongeza na janga la COVID-19 hali itakuwa mbaya zaidi.