Makaburi 6 ya umati yagunduliwa Niger, yana maiti za makumi ya raia
(last modified Sat, 05 Sep 2020 07:14:05 GMT )
Sep 05, 2020 07:14 UTC
  • Makaburi 6 ya umati yagunduliwa Niger, yana maiti za makumi ya raia

Afisa wa shirika moja lisilo la serikali nchini Niger amesema kuwa kumegunduliwa makaburi sita ya umati yenye maiti za karibu watu 71 wanaodaiwa kuuliwa na wanajeshi wa serikali katika eneo la Tillabéri magharibi mwa Niger.

Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali linaloshiriki katika uchunguzi wa Kamisheni ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Niger, Abdullah Sido amesema kuwa baadhi ya wanajeshi wa serikali wanaoshiriki katika operesheni ya kupambana na makundi ya kigaidi wamehusika na mauaji ya kiholela ya makumi ya raia katika eneo la Tillabéri.

Abdullah Sido ameongeza kuwa, habari ya kuuliwa makumi ya raia ambao hawakuwa na silaha ni ya kweli, na kwamba maiti za watu wasiopungua 71 waliouawa na askari hao zimepatika katika makaburi sita ya umati. 

Amesema kuwa wanajeshi na askari usalama wa taifa ndio waliohusika na mauaji hayo ya holela. 

Katika miezi ya hivi karibuni maeneo ya magharibi mwa Niger yamekuwa yakisumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya kigaidi. 

Mwaka jana wa 2019 makundi hayo yalishambulia kambi kadhaa za jeshi la taifa huko magharibi mwa Niger na kuuwa watu wasiopungua 14.  

Tags