Wapinzani waendelea kupinga Ouattara kugombea tena urais Ivory Coast
Wapinzani nchini Kodivaa wamendelea kupinga na kulalamikia hatua ya Rais Alassane Outtara ya kuamua kugombea tena urais nchini humo.
Televisheni ya "France24" imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wagombea 44 wa urais wamepasishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea urais nchini Ivory Coast akiwemo Rais Ouattara. Hata hivyo, Pascal Affi N'Guessan, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo wa wakati wa utawala wa Laurent Gbagbo kutoka chama Harakati ya Wananchi amemuwekea pingamizi Ouattara.
Katika upande mwingine, Charles Blé Goudé, mkuu wa zamani wa chama cha Vijana Wazalendo, hivi sasa anafanya juhudi za kuhakikisha uchaguzi huo unaakhirishwa.
Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Kodivaa pamoja na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo, hadi hivi sasa wanaendelea kupinga kuakhirishwa uchaguzi huo.
Ni vyema kusema hapa kwamba Katiba ya Ivory Coast ya mwaka 2016 ilibana kipindi cha mtu kugombea urais. Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya katiba, mtu haruhusiwi kugombea urais kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano mitano.
Hata hivyo wafuasi wa Rais Alassane Ouattara wanasema kuwa, marekebisho ya Katiba ya mwaka 2016 yalifuta yote yaliyopita kabla ya hapo kwa maana kwamba Ouattara sasa hivi anahesabiwa kama vile hajawahi kugombea urais hata mara moja. Madai hayo yanapingwa na wapinzani na baadhi ya wanasheria ambao wanasema kuwa, kugombea tena urais Alassane Ouattara ni kinyume cha sheria.
Uchaguzi wa Rais unatarajiwa kufanyika tarehe 31 mwezi ujao wa Oktoba katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye historia ya machafuko ya uchaguzi.