Watu 58 wauawa katika mashambulizi ya ADF mashariki mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63352-watu_58_wauawa_katika_mashambulizi_ya_adf_mashariki_mwa_kongo_dr
Watu wasiopungua 58 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio ya wanamgambo wa ADF wa Uganda katika mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 11, 2020 02:42 UTC
  • Watu 58 wauawa katika mashambulizi ya ADF mashariki mwa Kongo DR

Watu wasiopungua 58 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio ya wanamgambo wa ADF wa Uganda katika mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yameelezwa na Adjio Gidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC na kuongeza kuwa, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyoshambuliwa wamekimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.

Amesema, "ADF iliua watu 23 katika eneo la Irumu kusini mwa mkoa wa Ituri Jumanne na kisha ikaua watu wengine 35 katika eneo hilo siku iliyofuatia. Vikosi vyetu vimeshafika katika maeneo hayo kukabiliana na wanamgambo hao."

Mmoja wa wakazi wa kijiji chenye misitu mikubwa cha Tshabi mkoani hapo amenukuliwa na duru za habari akisema kuwa, wanamgambo hao walitumia bunduki, visu, mapanga na silaha nyinginezo katika mashambulio hayo ya Jumanne na Jumatano. 

Wanamgambo wa ADF

Mapema mwezi Juni mwaka huu, watu 16 waliuawa na ADF mkoani Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwemo watoto 5 wa kike; wiki chache baada ya genge hilo kuua watu wengine 17 katika hujuma tofauti mkoani hapo.

Maelfu ya Wakongomani wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi, tokeo mwaka 2014. 

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.