Magufuli asikitishwa na 'ajali' ya moto iliyoua wanafunzi 10 Tanzania
(last modified Tue, 15 Sep 2020 07:48:11 GMT )
Sep 15, 2020 07:48 UTC
  • Magufuli asikitishwa na 'ajali' ya moto iliyoua wanafunzi 10 Tanzania

Rais John Magufuli wa Tanzania ametuma salamu za rambirambi kwa uongozi wa Shule ya Kiislamu ya Byamungu iliyopo wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kufuatia mkasa wa moto uliosababisha maafa. Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa wanafunzi 10 waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya usiku wa kuamkia jana.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni jana Jumatatu, Rais Magufuli alisema, “Nimesikitika sana na taarifa za watoto 10 kufariki kwa moto shuleni Byamungu, naombeni wote tusimame tuziombee roho za marehemu zipumzike kwa amani."

Wanafunzi hao walifariki dunia huku makumi ya wengine wakijeruhiwa baada ya moto kuunguza bweni moja katika shule ya msingi ya wavulana iliyoko katika kijiji cha Itera, wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, kaskazini magharini mwa Tanzania.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia jenerali Marco Gaguti amethibitisha kutokea mkasa huo na kusema, moto huo ulitokea Jumapili usiku saa tano kwa saa za huko, na kuunguza bweni hilo lililokuwa na wanafunzi 74. Ameongeza kuwa, wanafunzi wengi waliokwama ndani ya bweni hilo waliokolewa na polisi, kikosi cha uokoaji, na watu wanaoishi jirani na shule hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, lakini ameunda kamati ya uchunguzi, ambayo anatumai kuwa itagundua chanzo cha moto huo.

Tanzania katika siku za hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la ajali za moto katika shule za nchi hiyo hususan za Kiislamu.