Wahajiri 8 wa Ethiopia wafariki katika pwani ya Djibouti
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema wahajiri wasiopungua 8 kutoka Ethiopia wamezama baharini na wengine 12 wametoweka baada ya wafanya magendo ya binadamu kuwarusha baharini karibu na Pwani ya Djibouti.
Taarifa ya IOM imesema wahajiri wengine 14 wamenusurika na sasa wanapata matibabu. Inaaminika kuwa wahajiri hao walikuwa wanataka kupitia Djibouti wakialekea Yemen kwa lengo la kuingia katika nchi za Ghuba ya Uajemi kutafuta ajira. Duru zinaarifu kuwa wahajiri waliotupwa baharini ni wanawake na watoto.
IOM inasema katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, wahajiri 2,000 wamewasili Djibouti wakitokea Yemen lakini pamoja na hayo, bado kuna wahajiri wanaoelekea Yemen.
Hayo yanajiri wakati ambao hivi karibuni, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitangaza habari ya kupoteza maisha wahamiaji watatu wa Kiethiopia ambao walikuwa wanashikiliwa katika mazingira yasiyo ya kibinadamu nchini Saudi Arabia.

Ripoti iliyotolewa Ijumaa na shirika hilo imesema maelfu ya wahajiri hao wa Kiethiopia wanapitia kipindi kigumu katika vituo vya kuwazuilia nchini Saudia, na hali imekuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha janga la corona.
Mtafiti wa Amnesty International, Marie Forestier amesema katika taarifa kuwa, "maelfu ya raia wa Ethiopia walielekea Saudi Arabia kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri, lakini badala yake wamekumbana na hali ngumu na isiyo ya kibinadamu."
Ameitaka serikali ya Riyadh iwaachie huru wahajiri inayowazuilia kinyume cha sheria, na vile vile iboreshe hali ya kambi inazotumia kuwazuilia wahamiaji hao.