Jinai mpya ya Boko Haram, muendelezo wa misimamo ya kufurutu ada Afrika
(last modified Mon, 30 Nov 2020 13:14:05 GMT )
Nov 30, 2020 13:14 UTC
  • Jinai mpya ya Boko Haram, muendelezo wa misimamo ya kufurutu ada Afrika

Baada ya makundi ya kigaidi kudhoofishwa katika maeneo mbali mbali ya Asia Magharibi, hivi sasa makundi hayo yameeneza satwa yao na kuimarika katika maeneo mbali ya barani Afrika ambapo yamekithirisha hujuma. Katika tukio la hivi karibuni, magaidi wakufurishaji wa Boko Haram wameua wakulima 110 katika kijiji cha Koshobe karibu na Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno ambalo ni kitovu cha magaidi hao, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Mauaji hayo ya umati yamejiri sambamba na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umekuwa ukiakhirishwa katika jimbo hilo mara kwa mara kutokana na hujuma za Boko Haram zilizoanza mwaka 2009.

Harakati za makundi ya kigaidi zimeongezeka sana katika eneo la magharibi mwa Afrika hasa katika eneo la ukanda wa Sahel. Makundi makubwa zaidi ya kigaidi katika eneo hilo ni Boko Haram na ISIS au DAESH.

Ongezeko la harakati za makundi ya kigaidi katika eneo hilo linaweza kuangaziwa kwa mitazamo kadhaa. 

Pamoja na kuwepo madai ya baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika Magharibi, hasa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, kuhusu azma ya kupambana na kuangamiza magaidi, lakini hakuna hatua za kivitendo zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.

Ukosefu wa bajeti, kutokuwa na vikosi vya usalama vyenye uwezo na ujuzi wa kutosha, hitilafu za ndani ya nchi, matatizo ya kiuchumi, umasikini, ukosefu wa ajira na mivutano ya nyuma ya pazia na ufisadi, ni mambo ambayo yamepelekea  makundi kama vile Boko Haram kupanua wigo wa ugaidi katika eneo hilo.

Hali kadhalika ongezeko la uingiliaji wa madola ajinabi katika eneo  ni sababu nyingine ya kushadidi ugaidi magharibi mwa Afrika. Jitihada za baadhi ya tawala hasa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni za kutaka kujipenyeza katika eneo hilo kumepelekea tawala hizo mbili zimimine silaha kwa serikali tegemezi za eneo hilo. Lakini ukweli ni kuwa tawala hizo mbili pia zimekuwa zikiwafikishia magaidi silaha kwa siri.

Katika upande wa pili,  matatizo ya kiuchumi katika nchi za Afrika yamepelekea makundi ya kigaidi yaweze kuwavutia vijana wasiokuwa na ajira na ambao wamepoteza matumaini maishani.

Weledi wa mambo ya kisiasa wanasema ukosefu wa usalama katika mipaka, ongezeko la umasikini, kuenea jangwa, ukosefu wa maji na hitilafu za kikabila katika maeneo ya kilimo ni kati ya sababu muhimu za kuenea makundi ya magaidi wakufurishaji barani Afrika.

Pigo kubwa ambalo makundi ya kigaidi, hasa ISIS, yamepata Syria na Iraq ni jambo ambalo limepelekea makundi hayo yatafute maeneo mapya ya kueneza satwa yao barani Afrika. Makundi hayo ya kigaidi yamehamishia baadhi ya wapiganaji wao barani Afrika.

Katika upande mwingine, migogoro ya kisiasa na kiuchumi katika nchi kama vile Libya, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Msumbiji na Mali ni fursa ambayo imetoa mwanya kwa magaidi kujipenyeza.

Naqi al Najar, mtaalamu wa masuala ya usalama katika Kituo cha Utafiti wa Kistratijia Misri anasema: 'Baada ya ISIS kupata pigo Syria na Iraq sasa imeelekeza nguvu zake barani Afrika na inachochea ugaidi na misimamo mikali katika bara hilo."

Inaelekea kuwa, iwapo wakuu wa nchi husika za Afrika hawatachukua hatua imara kukabiliana na magaidi basi bara hilo litageuka kuwa uwanja mkubwa wa magaidi. Nchi za Afrika hazipaswi kusubiri misaada ya madola ya Magharibi ili kufanikisha vita dhidi ya ugaidi kwani nchi hizo zenyewe sasa zinakumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Isisahaulike kuwa ukosefu wa usalama barani Afrika pia huwezesha madola ya kibeberu ya nchi za Magharibi kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo na kuendeleza uporaji wa utajiri wa nchi hizo.