Watu watano wauawa katika hujuma ya kigaidi Dhobley, Somalia
(last modified Wed, 30 Dec 2020 04:33:02 GMT )
Dec 30, 2020 04:33 UTC
  • Watu watano wauawa katika hujuma ya kigaidi Dhobley, Somalia

Watu watano wameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa kwenye mlipuko uliojiri kwenye barabara ya mji wa Dhobley katika mkoa wa Lower Juba kusini mwa Somalia.

Gavana wa mji wa Dhoblye Bw. Mohamed Hassan amesema  Jumanne kuwa mlipuko huo wa Jumatatu ulikuwa ni bomu la kutegwa ardhini ambalo lililenga basi lililokuwa linapita. Watu watano waliokuwa kwenye basi hilo waliuawa papo hapo, na wapita njia wengine wawili walijeruhiwa.

Mpaka sasa hakuna aliyetangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini huko nyuma kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye uhusiano na kundi la Al-Qaeda limewahi kudai kuhusika na mashambulizi kama hayo.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la Al-Shabaab limekuwa likiendesha harakati za mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia. 

Mwaka 2011, jeshi la Somalia likisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyojulikana kama AMISOM lilifanikiwa kuwatimua magaidi wa Ash-Shabaab katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Hata hivyo kundi hilo la kigaidi lingali linayadhibiti maeneo mengi ya vijijini ya nchi hiyo.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

 

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

Tags