Wanajeshi kadhaa wa Misri wauawa na kujeruhiwa kaskazini mwa nchi
Wanajeshi wasiopungua wanane wa Misri wameuawa na kujeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga bomu katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Duru za kiusalama za Misri zimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, jana usiku gari la wanajeshi wa nchi hiyo lilikokuwa linapiga doria huko Sinai Kaskazini lilikanyaga bomu la kutegwa ardhini na kusababisha wanajeshi watatu kuuawa na wengine watano kujeruhiwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, jeshi hilo la Misri lilikuwa linapiga doria katika eneo lijulakano kwa jina la Bi'ir al 'Abd, katika mkoa huo wa kaskazini mwa Misri, wakati lilipokanyaga bomu na kuripuka.
Rasi ya Sinai ya kaskazini mwa Misri, imekuwa ni maficho makubwa ya magenge ya kigaidi tangu mwaka 2015 kutokana na muundo wake maalumu wa kijiografia.
Jeshi la Misri lilitangaza vita vya pande zote dhidi ya genge la kigaidi na ukufurishaji la Ansar Bayt al Muqaddas hasa baada ya genge hilo kutangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la ISIS.
Jeshi la Misri limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na magenge hayo ya kigaidi katika rasi ya Sinai.
Ijapokuwa ngome kuu ya magaidi hao ni mkoa wa Sinai Kaskazini, lakini mara kwa mara magenge ya magaidi hao yanafanya mashamblizi katika meneo mengine ya Misri ikiwemo kusini mwa Sinai.
Genge linalojiita Ansar Bayt al Muqaddas ndilo hatari zaidi katika rasi ya Sinai ambapo baada ya kutangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh, lilibadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.