Wanamgambo wa ADF waua raia wengine 22 Kongo DR
Watu wasiopungua 22 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika mkoa wa Kivu Kaskazini huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Donat Kibwana, afisa wa utawala wa eneo la Beni mkoani hapo aliliambia shirika la habari la Anadolu jana Jumatano kuwa, wapiganaji hao wa ADF walivamia kijiji cha Mwenda usiku wa kuamkia Jumanne, na kuua raia wasiopungua 22 kwa kutumia mapanga.
Naye Fulbert Kasairo, afisa wa serikali katika eneo la Beni amesema mbali na kutekeleza mauaji hayo ya kutisha, wanamgambo hao waliwaibia wakazi wa kijiji hicho.
Luteni Antony Mwalushayi wa Jeshi la Ulinzi la Kongo DR (FARDC) amethibitisha habari ya kutokea mauaji hayo, ingawaje hakutoa maelezo zaidi.
Ikumbukwe kuwa, usiku wa kuamkia mwaka mpya 2021, wanamgambo hao wa kundi la ADF wa Uganda walishambulia eneo la Beni katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini mashariki mwa DRC na kuua raia wasiopungua 25.
Kundi la hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Congo DR tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.