Bara la Afrika kuagiza dozi milioni 300 za COVID-19, maambukizi yaongezeka
Umoja wa Afrika umeazimia kuagiza dozi milioni 300 za chanjo ya COVID-19 , huku maambukizi ya ugonjwa huo yakiongezeka barani humo.
Nicaise Ndembi, mshauri mkuu wa masuala ya kisayansi katika kituo cha Umoja wa Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa, Africa-CDC ameongeza kuwa makubaliano ya upatikanaji chanjo hizo yatakuwa ni makubwa zaidi ya aina yake barani Afrika.
Ndembi ameongeza kuwa dozi hizo milioni 300 ni kutokana na juhudi binafsi za kampuni ya COVAX, kwa lengo la kupelekwa kwenye nchi zenye mapato ya chini.
Hayo yanajiri wakati ambao maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika yamepindukia watu milioni tatu. Afrika Kusini ndiyo iliyoathirika zaidi barani Afrika ikiwa imerekodi zaidi ya maambukizi milioni 1.2. Taasisi ya Afrika ya kudhibiti maaradhi ya kuambukiza imesema jumla ya dozi bilioni 1.5 za chanjo ya COVID-19 zinahitajika Afrika na inakadiriwa kuwa zitagharimu dola bilioni 10.
Hayo yanajiri wakati ambao, Rais Lazarus Chakwera wa Malawi jana alitangaza janga la kitaifa kutokana na kuongezeka kwa kasi maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo.
Katika hotuba maalumu kwa taifa, Rais Chakwera amesema, kufuatia ongezeko kubwa la vifo na maambukizi mapya ya virusi vya Corona, ataitisha mkutano wa dharua kujadili hatua zijazo za kinga na udhibiti.
Pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza misaada kwa Malawi ili kuisaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na janga la COVID-19.