Jan 17, 2021 08:00 UTC
  • ISIS yadai kuhusika na kutekwa kambi ya jeshi Nigeria

Maafisa usalama na mamia ya wakazi wa mji mmoja katika jimbo la Borno la kaskazini mwa Nigeria wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya genge la magaidi waliojizatiti kwa silaha kushambulia na kudhibiti kambi ya jeshi katika eneo hilo.

Wapiganaji wa genge la ISIS katika eneo Afrika Magharibi  (ISWAP) walishambulia kambi hiyo ya jeshi iliyoko katika mji wa  Marte katika eneo la Ziwa Chad jimboni Borno, baada ya kujiri mapigano makali baina yao na wanajeshi wa Nigeria.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, makabiliano hayo baina ya magaidi na askari wa Nigeria yalifanyika usiku kucha Ijumaa na yakaendelea hadi jana Jumamosi. 

Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema askari hao wa serikali hawakumbia kambini hapo, bali waliondoka kama moja ya stratejia ya vita ili wajipange upya kuwashambulia magaidi hao waliojizatiti kwa silaha.

Kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) kupitia shirika lake la habari za kipropaganda la Amaq na kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii limekiri kuhusika na shambulio hilo. Haijabainika idadi ya waliojeruhiwa au kuuawa katika shambulio hilo la kigaidi.

Magaidi wa Boko Haram

Hata hivyo, Benard Onyeuko, Msemaji wa Jeshi la Nigeria katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la Xinhua kuwa, idadi kubwa ya magaidi wa Boko Haram wameuawa katika mapigano hayo.

Shambulio hilo dhidi ya jeshi la Nigeria linajiri siku chache tu baada ya maafisa usalama 11 wakiwemo wanajeshi wanne kuuawa katika shambulio la bomu la kutegwa ardhini la kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo hilo la Borno huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Tags