Feb 13, 2021 08:46 UTC
  • Kesi ya tatu ya Ebola yathibitishwa DRC huku watu 200 wakifuatiliwa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha kesi ya tatu ya ugonjwa wa Ebola katika mji wa Butembo jimboni Kivu Kaskazini, eneo ambalo lilikuwa kitovu cha mlipuko wa 10 wa ugonjwa huo uliotangazwa kumalizika mwezi Juni mwaka jana.

Eugene Nzanzu Salita, Waziri wa Afya katika jimbo hilo amesema wanawafuatilia watu 200 wanaoaminika kuwa walitagusana na watu watatu waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huo kufikia sasa.

Ameongeza kuwa, dozi 1,200 za chanjo ya Ebola ziliwasili nchini humo jana Ijumaa pamoja na wataalamu kadhaa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wanaotazamiwa kusaidiana na wahudumu wa afya wa DRC katika kampeni ya kuwachanja wakazi wa eneo hilo.

DRC iliripoti kesi ya kwanza ya Ebola Jumapili iliyopita, miezi miwili baada ya WHO kutangaza mlipuko wa 11 wa maradhi hayo katika mkoa wa Équateur, magharibi mwa nchi.

Wakazi wa Butembo wakipigwa chanjo ya Ebola

Mlipuko wa 10 wa Ebola nchini DRC ulidumu kwa takribani miaka miwili na ulikuwa mlipuko wa pili kwa ukubwa duniani ukiwa na wagonjwa 3481 ambapo kati yao hao 2299 walifariki dunia na 1162 walipona. Harakati za kukabili mlipuko huo zilikuwa zinakumbwa na changamoto kutokana na ukosefu wa usalama kwenye eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.

Tags