Mar 01, 2021 12:25 UTC
  • UN: Ufisadi wa fedha umejiri katika kumchagua Waziri Mkuu wa Libya

Ripoti ya Wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, rushwa ya fedha ilitolewa kwa watu wasiopungua 3 ambao ni wajumbe wa kikao cha mazungumzo ya kisiasa ya Libya katika kumchagua Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameandaa ripoti kuhusu kununuliwa kura za wajumbe wasiopungua watatu wa kikao cha mazungumzo ya kisiasa ya Libya; ambapo Abdulhamid al Dadaiba alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. 

Kupitia ripoti hiyo, wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamebaini kuwa, katika kikao cha mazungumzo ya kisiasa ya Libya huko Tunis mji mkuu wa Tunisia wajumbe wawili wa kikao hicho walilipwa dola 150,000 huku mjumbe wa tatu pia akipatiwa dola 200,000 ili kumpigia kura Abdulhamid al Dadaiba ili awe Waziri Mkuu wa Libya. 

Imeelezwa kuwa, Waziri Mkuu huyo wa Libya aliyechaguliwa hivi karibuni ni mmoja wa wawekezaji wakuu nchini humo. 

Ripoti hii ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inatazamiwa kuwasilishwa kwa Baraza la Usalama la umoja huo mwezi huu.

Itakumbukwa kuwa, Baraza la Mazungumzo ya Libya lililoandaa kikao chake huko Geneva chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa lilimchagua Abdulhamid al-Dabaiba kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, Mohamed Yunus al-Menfi kuwa Mkuu wa Baraza la Urais, na Abdullah Hussein Al Lafi na Musa Al Koni kuwa wajumbe wawili wa baraza hilo ili kuandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi wa rais na bunge mwezi septemba mwaka huu.  

Abdulhamid al-Dabaiba (kushoto),  Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya , na Mohamed Yunus al-Menfi Mkuu wa Baraza la Urais

 

Tags