Wapinzani wenye silaha waondoka katika maeneo yao Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67716-wapinzani_wenye_silaha_waondoka_katika_maeneo_yao_sudan_kusini
Wapinzani wenye silaha huko Sudan Kusini wameondoka katika maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 10, 2021 07:10 UTC
  • Wapinzani wenye silaha waondoka katika maeneo yao Sudan Kusini

Wapinzani wenye silaha huko Sudan Kusini wameondoka katika maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya nchi hiyo.

Riek Machar, mkuu wa waasi waliokuwa wanaipinga serikali ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, ametoa amri kwa watawala wa kijeshi wa maeneo yanayodhibitiwa na kundi lake, waweke chini silaha na wachague viongozi wapya kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyokomesha mgogoro wa miaka mingi wa Sudan Kusini.

Amesisitiza kuwa, alilazimika kuchagua viongozi wa kuendesha na kusimamia maeneo hayo ili kujaza pengo la uongozi na masuala ya usalama kutokana na kutokuweko wakuu wa majimbo na wa mikoa. Hata hivyo sasa hivi na baada ya kufikiwa makubaliano ya amani na kuundwa serikali ya mseto, inabidi majimbo na mikoa hiyo ifuate makubaliano ya amani ya nchi hiyo.

Riek Machar (kulia) na Salva Kiir

 

Makubaliano ya amani ya Sudan Kusini yaliyomaliza mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo, yalifikiwa miaka miwili iliyopita baina ya Rais Salva Kiir na hasimu wake, Riek Machar.

Majimbo ya Upper Nile, Bahr al Ghazal na Equatoria ndiyo mikoa ya Sudan Kusini ambayo wapinzani wa serikali ya nchi hiyo wanaendesha mambo yao nje ya udhibiti wa Juba.

Mwezi Septemba 2018, pande hasimu nchini Sudan Kusini zilitiliana saini makubaliano ya amani huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Makubaliano hayo yalitaka kuundwe serikali ya mpito itakayoshirikisha vyama vyote na hilo lilifanyika mwezi Februari mwaka huu. Vipengee vingine ni pamoja na kulindwa umoja wa ardhi ya nchi hiyo na maeneo yote kuwa chini ya serikali kuu.