Somalia yachunguza madai ya kutumiwa watoto kama majasusi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6787-somalia_yachunguza_madai_ya_kutumiwa_watoto_kama_majasusi
Serikali ya Somalia imeanza kuchunguza madai kuwa vyombo vya usalama nchini humo vinatumia watoto wadogo kama majasusi na kuhatarisha maisha yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2016 02:47 UTC
  • Somalia yachunguza madai ya kutumiwa watoto kama majasusi

Serikali ya Somalia imeanza kuchunguza madai kuwa vyombo vya usalama nchini humo vinatumia watoto wadogo kama majasusi na kuhatarisha maisha yao.

Omar Abdirashid Sharmarke, Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema tayari wamebuni jopo la mawaziri wanne litakalochunguza madai hayo ambayo yalichapishwa hivi karibuni na gazeti la Washington Post.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, watoto wadogo na vijana ambao wameasi kundi la wanamgambo wa al-Shabaab wanatumiwa na Idara ya Kiintelijensia na Usalama wa Taifa ya nchi hiyo kama majasusi.

Waziri Mkuu wa Somalia ameongeza kuwa, serikali ya federali ya nchi hiyo imekuwa ikitoa msahama kwa mtu yeyote anayejisalimisha na kuasi makundi ya kigaidi likiwemo kundi la al-Shabaab.

Amesisitiza kuwa, watoto wadogo na vijana ambao wanaasi makundi hayo ya kigaidi hudhaminiwa usalama, kupewa ushauri-nasaha na kuelekezwa jinsi ya kutangamana tena na jamii.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likiwahadaa watoto na mabarobaro kujiunga nalo na kisha kuwatumia kama washambuliaji wa kujitolea muhanga.