UN: Zaidi ya 200 wameuawa katika mashambulio ya wabeba silaha DRC
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya 200 wameuawa katika mashambulio ya magenge ya wabeba silaha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tokea Januari mwaka huu hadi sasa.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la umoja huo (UNHCR) limeeleza kusikitishwa kwake na kushtadi wimbi la mashambulizi ya waasi na magenge ya wabeba silaha nchini humo.
Taarifa ya UNHCR imebainisha kuwa, mbali na mamia ya watu kuuawa tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, wengine zaidi ya 40,000 wamefurushwa kwenye makazi yao na hivi sasa wanaishi kama wakimbizi ndani na nje ya Kongo DR.
UNCHR imeongeza kuwa, akthari ya magenge hayo ya wabeba silaha yana mfungamano ama na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) au lile la ADF lenye asili ya Uganda.
Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, katika kipindi cha chini ya miezi mitatu iliyopita, wapiganaji wa ADF ambao mwaka jana waliua watu zaidi ya 465, wameshambulia vijiji 25 na kuchoma moto makumi ya nyumba mbali na kuteka nyara watu zaidi ya 70 mashariki mwa DRC.
Eneo la mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.