Al Azhar kuasisi asasi ya kukurubisha madhehebu ya Kiislamu Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6961-al_azhar_kuasisi_asasi_ya_kukurubisha_madhehebu_ya_kiislamu_misri
Mhadhiri mmoja wa fikihi katika Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri ametangaza habari ya kuasisiwa taasisi maalumu ya kukurubisha madhehebu ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2016 23:41 UTC
  • Al Azhar kuasisi asasi ya kukurubisha madhehebu ya Kiislamu Misri

Mhadhiri mmoja wa fikihi katika Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri ametangaza habari ya kuasisiwa taasisi maalumu ya kukurubisha madhehebu ya Kiislamu.

Shirika la habari la IQNA limeripoti habari hiyo na kumnukuu Sheikh Ahmed Karima, mhadhiri wa fikihi na sheria ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha al Azhar akisema leo Alkhamisi kuwa, iwapo madhehebu mbalimbali ya Kiislamu yatakurubiana na kudumisha umoja baina yao, itakuwa rahisi kutekelezwa sheria tukufu za Uislamu na kupatikana umoja kati ya Waislamu wote.

Amesema karibuni hivi kutaanzishwa taasisi maalumu ya kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu nchini humo. Amesema, maulamaa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha al Azhar ndio watakaoasisi taasisi hiyo. Hata hivyo amekataa kutangaza majina ya maulamaa na wanafunzi wa kidini watakaounda taasisi hiyo.

Sheikh Ahmed Karima, ni miongoni mwa maulamaa walio mstari wa mbele katika kupigania umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Aliwahi kunukuliwa akiwashukuru Waislamu wa Kishia nchini Iran kwa kuishi kwa salama na amani na ndugu zao wa Kisuni na kumshukuru pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwa uungwana wake mkubwa katika suala hilo.

Shirika la habari la Tasnim liliwahi kumnukuu Sheikh Ahmed Karima akisema: Ameshuhudia kwa macho yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akigharamia kifedha madrasa na shule za kidini za Kisuni katika mkoa wa Kurdistan kwa ajili ya kueneza mafundisho ya Waislamu wa madhehebu ya Kisuni nchini Iran. Alimshukuru pia Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa fatwa yake maarufu ya kuharamisha kuvunjiwa heshima maswahaba na wake wa Bwana Mtume Muhammad SAW.