Marais 11 wa nchi za Afrika wahudhuria hafla ya kuapishwa Rais Museveni wa Uganda
(last modified Wed, 12 May 2021 11:22:31 GMT )
May 12, 2021 11:22 UTC
  • Marais 11 wa nchi za Afrika wahudhuria hafla ya kuapishwa Rais Museveni wa Uganda

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameapishwa leo na kuanza rasmi kuongoza muhla wa sita baada ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Januari 14 mwaka huu.

Rais Museveni (76) amesema: Mimi Yoweri Kaguta Tibuhaburwa Museveni, naapa kwamba, nitaheshimu na kulinda sheria na kuwaleta wananchi wa Uganda ustawi na maendeleo."Museveni ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986 alishinda uchaguzi wa Januari 14 mwaka huu uliolalamikiwa na wapinzani kwa kupata asilimia 58 huku mpinzani wake mkuu Robert Kagulanyi mashuhuri kwa jina la Bobi Wine akipata asimilia 34 ya kura.

Kwa akali viongozi kutoka mataifa 11 barani Afrika wameshiriki katika hafla ya leo ya kuapishwa Rais Museveni.

Miongoni mwa Marais waliohudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Museveni ni Évariste Ndayishimiye  wa Burundi, Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Emmerson Mnangagwa Zimbabwe, Salva Kiir Sudan Kusini, Hage Gottfried Geingob wa Namibia na Alpha Conde wa Guinea.  

Baadhi ya viongozi wakiwasili Uganda kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni

 

Wengine ni Marais Felix  Tshisekedi wa Jamahuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nana Akufo-Addo wa Ghana, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya.  Wapinzani nchini Uganda wamesusia sherehe hizo za kuapisishwa Rais Museveni.

 Nyumba za viongozi wa upinzani Dakta Kizza Besigye na Bobi Wine mapema leo zilizingirwa na vikosi vya usalama baada ya kuripotiwa taarifa kwamba, baadhi ya wapinzani wanataka kuvuruga hafla ya kuapishwa Rais Museveni.

Aidha usalama uliimarishwa mno mapema leo katika jiji la Kampala ili kuwa tayari kukabiliana na hatua yoyote ya kutaka kuvuruga hafla hiyo.