Magaidi 100 wa al Shabab wauawa kusini mwa Somalia
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, limeua wanamgambo 100 wa genge la kigaidi la al Shabab wakiwemo makamanda kadhaa wa genge hilo katika operesheni maalumu ya kijeshi huko kusini mwa Somalia.
Mkuu wa majeshi ya Somalia, Brigedia Jenerali Odowaa Yuusuf Raage ameiambia redio ya Sauti ya Jeshi ya nchi hiyo kwamba jeshi la Somalia jana lilifanya operesheni kubwa dhidi ya magaidi wa al Shabab katika vijiji na maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shabelle na kuangamiza idadi kubwa ya magaidi wa al Shabab.
Jenerali Raageh hakutoa ufafanuzi mkubwa kuhusu operesheni hiyo ya kijeshi zaidi ya kusema kuwa, katika operesheni hiyo, makamanda kadhaa wa al Shabab na wanamgambo wengine wameangamizwa na jeshi la Somalia.
Mkuu huyo wa vikosi vya ulinzi vya Somalia vile vile amesema, jeshi la nchi hiyo limeteka pia zana za kijeshi pamoja na magari ya deraya ya magaidi wa al Shabab.
Aidha amesema, operesheni za jeshi la Somalia zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hadi yatakaposafishwa kikamilifu na uwepo wa magaidi.
Genge la al Shabab halijasema chochote kuhusu matamshi ya Mkuu wa Majeshi ya Somalia wala suala la kuuawa idadi hiyo kubwa ya wanamgambo wa genge hilo.
Genge la al Shabab lilianzishwa nchini Somalia mwaka 2004 na tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja. Idadi ya wanamgambo wa al Shabab mwaka 2014 ilikisiwa kuwa ni kati ya 7,000 hadi 9,000.