Sudan Kusini inakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2021
(last modified Thu, 03 Jun 2021 03:55:44 GMT )
Jun 03, 2021 03:55 UTC
  • Sudan Kusini inakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2021

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema upungufu mkubwa wa nafaka unatarajiwa nchini Sudan Kusini mwaka huu wa 2021, kutokana na athari za mgogoro wa muda mrefu na mafuriko.

Mashirika hayo yamesema hali hiyo imepelekea mamilioni ya Wasudan Kusini kuwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ripoti ya Tume ya Tathmini ya Usalama wa Mazao na Chakula iliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imesema upungufu wa chakula nchini Sudan Kusini unatarajiwa kufikia tani 465,600, ambacho ni kiwango cha juu mwaka huu.

Ripoti hiyo imesema uzalishaji wa chakula uliongezeka kwa asilimia saba mwaka 2020 ukifika tani 874,400, lakini ongezeko hilo linaweza kukidhi thuluthi moja tu ya mahitaji ya jumla ya watu milioni 12.2 wa Sudan Kusini, kwani nchi hiyo inahitaji tani milioni 1.3 za chakula kwa mwaka. Kwa msingi huo watu wengi Sudan Kusini wanategemea msaada wa chakula wa mashirika ya misaada ya kibinadamu ingawa nchi hiyo ina uwezo mkubwa wa kilimo.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Mashirika ya kutoa misaada yanasema watu milioni 7.9 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kuanzia Aprili hadi Julai. Mwakilishi wa FAO Sudan Kusini Meshack Malo anasema suluhisho la ukosefu wa chakula ni kupatikana amani ya kudumu nchini humo ili kuwawezesha Wasudani Kusini kufaidika na ardhi yao yenye rotuba na kuzalisha chakula cha kutosha na kuacha kutegemea misaada.