Jun 04, 2021 02:45 UTC
  • Jeshi la Nigeria laangamiza magaidi 50 wa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuangamiza magaidi wasiopungua 50 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Mohammed Yerima, Msemaji wa Jeshi la Nigeria alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, magaidi hao waliuawa baada ya askari wa nchi hiyo kutibua mashambulizi kadhaa ya wanamgambo hao katika mji wa Damboa jimboni Borno.

Amesema kikosi cha nchi kavu kilishirikiana na kile cha anga katika operesheni hiyo dhidi ya wanachama wa kundi hilo waliokuwa wamejizatiti kwa silaha huku wakitumia magari ya deraya yenye nambari feki za usajili pamoja na pikipiki.

Siku ya Jumatatu pia, magaidi 10 wa kundi hilo la ukufurishaji waliangamizwa kwenye operesheni iliyoendeshwa na jeshi la Nigeria katika mkoa wa Rann, katika jimbo hilo hilo la Borno.

Magaidi wa Boko Haram

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS). 

Mgogoro wa Boko Haram umeshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.

 

 

Tags